Kiungo Mshambuliaji wa mabingwa watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans, Maxi Nzengeli, amewataka wachezaji wenzake katika timu hiyo kusahau ushindi mnono wa mabao 5-1 walioupata dhidi ya watani zao Simba SC na badala yake waelekeze akili na nguvu kwenye michezo inayofuata.
Maxi amesema kuifunga Simba SC sio mwisho wa ligi kwani bado wana michezo mingi mbele yao ambayo wanatakiwa kufanya vizuri ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.
“Bado tuna michezo mingi mbele yetu, ni kweli tunafuraha sana kupata ushindi mzuri dhidi ya Simba SC, lakini mapambano bado yanaendelea, tunatakiwa sasa kuelekeza akili na nguvu katika michezo inayofuata, hatutakiwi kubweteka,” amesema winga huyo.
Ameongeza ushindi dhidi ya Simba SC unapaswa kuwaongezea morali na hali ya kupambana kuelekea michezo inayofuata ya ligi hiyo yenye timu 16.
“Kuwafunga wapinzani wako wakubwa katika mbio za ubingwa kunakuongezea hali ya kujiamini na kupambana zaidi, tulipata ushindi dhidi ya Azam FC na sasa dhidi ya Simba SC, hii kwetu itaongeza morali kwetu wachezaji.” amesema nyota huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Maxi alifunga mabao mawili huku mengine yakifungwa na Kennedy Musonda, Stephanie Aziz Ki na Pacome Zouzoua.
Kwa sasa Young Africans ina alama 24 zinazoiweka kileleni, ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 19 na Simba SC yenye alama 18 iko katika nafasi ya ya fasi ya tatu huku Mtibwa Sugar yenye alama tano inaburuza mkia.
Ligi Kuu Tanzania Bara ilitarajiwa kuendelea tena leo kwa Simba SC kuikaribisha Namungo FC kutoka Lindi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, mchezo wa kukamilisha mzunguuko wa tisa.