Imebainika kuwa Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Gamondi atamtumia Mkongomani Maxi Mpia Zengeli kucheza namba 10 na siyo winga tena katika kuelekea msimu ujao.

Mkongomani huyo aliyesajiliwa na timu hiyo kwenye usajili mkubwa uliofungwa usiku wa kuamkia jana Jumanne (Agosti Mosi) amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea Maniema FC ya DR Congo akisajiliwa kama winga na siyo kiungo.

Kitendo cha kubadilishiwa majukumu nyota huyo anayetabiriwa ndiye staa anayekuja katika kikosi hicho, kutawapa ugumu baadhi ya wachezaji wanaocheza nafasi hiyo ambao ni Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua mmoja atalazimika kutokea pembeni au benchi.

Taarifa kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo, ambayo wameiweka huko Kijiji cha Avic Town, Kigamboni Kocha Gamondi amevutiwa na kiwango kizuri cha Maxi hususan kwenye umiliki wa mpira, kunyang’anya mipira na kupiga pasi za mwisho.

Mtoa taarifa huyo aliongeza kuwa, kocha huyo ameonekana kumuandaa Maxi katika mazoezi yake kwa kumuongezea baadhi ya mbinu ili kuhakikisha anacheza vizuri zaidi.

“Gamondi tayari ameshapata kikosi chake cha kwanza atakachokitumia kwa ajili ya msimu ujao, amefanya maboresho makubwa ya kikosi hicho.

“Hiyo ni kutokana na maingizo ya baadhi ya wachezaji wapya ambao wamesajiliwa, na kati ya mchezaji ambaye amemfurahia ni Maxi ambaye alisajiliwa kucheza kama winga, lakini baada ya kumuangalia mazoezini akavutiwa naye na kumbadilishia majukumu.

“Kocha huyo ameonekana kumtumia kucheza namba 10 katika michezo mitatu ya kirafiki ambacho tumecheza ukiwemo dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, hivyo basi huenda Maxi atamtumia kucheza nafasi hiyo,” amesema mtoa taarifa huyo.

Gamondi hivi karibuni alizungumzia hilo la kukiandaa kikosi chake amesema kuwa: “Nipo naendelea kukiboresha kikosi chagu katika baadhi ya maeneo, kikubwa nimevutiwa na wachezaji wote ambao nimewakuta Young Africans, kikubwa ninahitaji ushindani kwa kila mchezaji.”

Harry Kane anasubiri muda wa kuondoka
Kocha Liverpool amkataa Kylian Mbappe