Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema anaamini timu yake itatinga Hatua ya Makundi ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na jukumu la kufikia malengo litaongozwa na nyota wake wawili, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua.
Al Merrikh ya Sudan inatarajia kuwakaribisha Young Africans katika mechi ya michuano hiyo itakayochezwa Septemba 16, mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.
Akizungumza jijini Dar es salaam Gamondi amesema wachezaji wake wamefanya mazoezi magumu katika juma hili ambayo yamesaidia kutambua kiwango cha kila mmoja wao huku akiamini Pacome na Nzengeli ndio wameshikilia moyo’ wa Young Africans kwa sasa.
Gamondi amesema mazoezi hayo yamewaimarisha na watarejea Uwanjani wakiwa bora na kuitumikia vyema klabu yao ili kupata matokeo chanya kwenye mechi zote watakazocheza.
“Nimeona uwezo wa Maxi, Zouzoua na wengine wamefanya vizuri katika mechi zilizopita na hata mazoezini, lakini ninahitaji wawe bora zaidi kuelekea mechi ijayo dhidi ya Al Merrikh.
Kabla ya kwenda Rwanda tutakuwa na mchezo mmoja wa kirafiki ambao tutaucheza leo Jumamosi (Septemba 09), naamini wachezaji wangu wanaendelea vizuri na tutafikia malengo yetu,” amesema Gamondi.
Kocha huyo alisema mechi ya kirafiki watakayocheza itamsaidia kuona maendeleo ya kikosi chake baada ya mazoezi makali ya wiki mbili.
“Ninaamini kwa asilimia 80 nyota wangu wameimarika, ninahitaji kikosi bora ambacho kitatoa ushindani katika kila mchezo. Mechi zote tunazocheza zina ushindani, hatudharau timu, tunataka kupambana ili kufikia malengo, lazima tujiimarishe, ameongeza Gamondi.
Katika kuwajenga nyota wake, juma hili Gamondi alikiongoza kikosi chake katika mazoezi ya ufukweni ili kuwatengenezea pumzi wakati juzi na jana walihamia katika mazoezi ya gym (asubuhi) na jioni walihamia uwanjani.
Young Africans ndio mabingwa watetezi na vinara katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo itaendelea tena kuanzia Septemba 15, mwaka huu baada ya kupisha kalenda ya kimataifa kumalizika.