Klabu ya Tanzania Prisons imeachana na Kocha Salum Shaban Mayanga kwa makubaliano ya kuvunja mkataba uliokua unaziunganisha pande hizo mbili.
Mayanga ameachana na Tanzania Prisons ambayo aliinoa kwa misimu miwili iliyopita, huku akiiwezesha timu hiyo kuwa miongoni mwa timu zilizoogopwa msimu uliopita.
Kikosi cha klabu hiyo ya Maafande wa Jeshi la Magereza kitakua chini ya Kocha Msaidizi Shaban Kazumba hadi Uongozi utakapomtangaza Kocha mpya.
Kuondoka kwa Mayanga kunaendelea kukoleza taarifa za kupewa majukumu ya kukinoa kikosi cha Mtibwa Sugar, ambacho kwa sasa hakina Kocha Mkuu kufutia kutimuliwa kwa Kocha Joseph Omog.
Mapema hii leo taarifa kutoka Manungu-Turiani mkoani Mororgoro zilieleza kuwa, Mayanga alionekana klabuni hapo saa chache baada ya kuthibitika Uongozi wa Mtibwa umeachana na Omog.
Endapo Mayanga atajiunga na Mtibwa Sugar, atakua anarudi nyumbani ambako aliacheza na kufundisha soka kwenye kikosi cha klabu hiyo, ambayo jana Jumapili (Desemba 12), ilipata ushindi wa kwanza msimu huu 2021-22 kwa kuifunga Biashara United Mara mabao 2-0.