Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Shabani Mayanga ametangaza kikosi kitakachocheza na Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa chini ya utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Wiki ya FIFA kwa mechi za kimataifa inatarajiwa kuanza Jumatatu Agosti 28 hadi Septemba 2, mwaka huu ambako Tanzania imekubaliana kucheza Botswana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Septemba 2, 2017.
Katika kikosi hicho cha wachezaji 21, Kocha Mayanga amemwita upya Mlinzi wa Young Africans, Kelvin Yondani huku nyota kutoka nje ya mipaka ya Tanzania wakiwa ni saba akiwamo nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Ally Samatta.
Kikosi hicho kinachotarajia kuingia kambini kesho Jumapili kuanzia saa 2.00 usiku ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).
Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).
Viungo ni Himid Mao – Nahodha Msaidizi (Azam FC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Saimon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (CD Tenerif/Hispania) na Orgenes Mollel (FC Famalicao/Ureno).
Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans), Kelvin Sabato (Azam FC), Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji) na Elias Maguli (Dhofar FC/Oman).
Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).