Mshambuliaji hatari wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele, ameweka hatima yake ya kuendelea kusalia ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa mashindano wa 2023/24 kuwa upo mikononi mwa viongozi wa klabu hiyo.
Mayele ameibuka kuwa miongoni mwa wa washambuliaji bora kwa sasa barani Afrika na ameweka rekodi nyingine ya kuwa mchezaji ambaye amefunga katika kila mashindano aliyocheza msimu huu kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.
Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo amekuwa na kiwango kizuri kwa msimu huu kwa kutwaa kiatu cha Ufungaji Bora Ligi Kuu Bara akishirikiana na kiungo wa Simba SC, Saido Ntibazonkiza baada ya kila mmoja kuweka nyavuni mabao 17, lakini Mkongomani huyo pia akionyesha ubora pia kwa kuwa kinara wa ufungaji kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika akimaliza na mabao saba.
Kiwango hicho kimemfanya Mayele kuhusishwa na kutakiwa na klabu mbalimbali ikiwamo Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo Kocha wake Nasreddine Nabi anatarajiwa kuifundisha msimu ujao, huku timu nyingine inayohitaji huduma yake ikitajwa kuwa ni Mamelodi Sundowns ya nchini humo.
Mayele amesema ana mkataba wa mwaka mmoja umesalia ndani ya klabu yake hiyo na tayari amepata ofa nyingi ambazo ziko mezani mwa viongozi wa timu yake hiyo zikihitaji huduma yake.
Amesema baada ya kumaliza majukumu ya timu ya Taifa anatarajia kukutana na viongozi wa timu yake kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ofa za klabu zilizomhitaji.
“Watu wanasubiri “Thank You’ ya kwangu ila hatima yangu ipo chini ya viongozi wa Young Africans, nilikuwa na majukumu na timu ya taifa, lakini sasa nimerudi Tanzania maana familia yangu iko hapa, najua watu wengi wanasubiri neno hilo ambalo kwa sasa limekuwa maarufu.
Ameongeza kuwa baada ya kumalizana na kujua hatima yake, ataenda visiwani Zanzibar kumsapoti mchezaji mwenzake wa zamani wa Young Africans, Feisal Salum Fei Toto’, ambaye ameandaa mechi kwa ajili ya kuwasaidia kinamama wajawazito.
“Nitaenda visiwani Zanzibar kucheza mechi Juni 24, mwaka huu katika Uwanja wa Mau Zedong na baada ya hapo nitaelekea Morogoro kwenye mechi ya hisani Juni 30, mwaka huu mchezo uliondaliwa na Shomari Kibwana na Dickson Job,” amesema Mayele huku akiwatania wachezaji wenzake hao kwa kudai kuwa atacheza timu ya yule atakayempa pesa nyingi kati ya Kibwana na Job kwa sababu anapenda sana pesa.