Aliyekuwa Mshambuliaji na Mfungaji Bora wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Fiston Kalala Mayele, amesema katika msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Pyramids FC ya Misri, ni kuhakikisha anafunga mabao zaidi ya kumi.
Mayele raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), aliondoka Young Africans mwishoni mwa msimu uliopita na kujiunga na Pyramids FC.
Akifanya mahojiano nchini Misri, Mayele amesema anahitaji kufanya vizuri zaidi msimu wake wa kwanza nchini humo anaamini atatimiza lengo lake kutokana na kujituma.
“Ukiacha kufunga pia nitatoa pasi za kutosha, naamini hakuna kinachoshindikana kila kitu ni maamuzi, nimecheza mechi tatu na nimefanikiwa kufunga bao moja,” amesema.
Mshambuliaji huyo amesema ligi ya Misri ni ngumu, kila timu inapoingia uwanjani inakuwa haijui itamalizaje mechi kutokana na ubora wa timu zote.
Amesema sababu ya ligi ya nchini humo kuwa namba moja Afrika ni ubora wa kila timu kuhakikisha inafanya vizuri katika kila mashindano.
“Ligi ya Misri ni ngumu, nilikuwa najiuliza ni kwa nini yenyewe ni bora kuliko Afrika nzima lakini sasa nimepata jibu, watu wameweka fedha zao na kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa na hakuna timu ambayo inaingia na matokeo uwanjani,” amesema.
Amesema aliikataa Al Ahly ya nchini humo kutokana na kuona ni timu yenye presha kubwa wakati Mamelodi Sandowns akihofia kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza kutokana na ubora wa washambuliaji waliokuwepo.
“Mamelodi ina washambuliaji wazuri na sikutaka kugawana nao mechi, leo nicheze na kesho nisicheze nikaona njia rahisi ni kwenda Pyramids ambayo nitacheza kwa kulinda kipaji changu,” amesema Mshambuliaji huyo.
Mayele aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, amesema lengo lake ni kuisadia timu yake kutwaa ubingwa wa michuano yoyote wanayoshiriki Msimu huu 2023/24.