Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele amesema, kikosi cha klabu hiyo hakina budi kupambana bila kuchoka katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Makundi, ili kitinge Hatua ya Robo Fainali.
Young Africans ilifanikiwa kufika Hatua ya Makundi kwa kuitoa Club Africain ya Tunisia iliyokubali kufungwa nyumbani kwao mjini Tunis 1-0, baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana jijini Dar es salaam mwaka 2022.
Mayele amesema lengo kuu ya Young Africans lilikuwa ni kutinga Hatua ya Makundi katika Michuano hiyo, sasa kilichopo ni kuhakikisha klabu yao inakuwa sehemu ya timu nane (8) zitakazocheza Robo Fainali msimu huu.
“Awali malengo ya timu yalikuwa ni kuhakikisha tunafika Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, tunashukuru tulifanikiwa hilo.”
“Baada ya kufikia lengo la kwanza, sasa lengo la pili ni kufika Hatua ya Robo Fainali, tunafahamu ni jinsi gani kuna changamoto ya ushindani kufikia hatua hiyo, lakini tuna sababu ya kuendelea kupambana na tunaamini tutaendelea kufanikiwa.”
“Sina Presha kubwa kwa kuwa nimewahi kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, hivyo ninatamani kuona nikiisaidia Young Africans kufikia hatua hiyo.” amesema Mayele
Young Africans itaanza kampeni ya kucheza Robo Fainali ya Michuano hiyo Febriari 12 mjini Tunis-Tunisia kwa kupapatuana na US Monastir, huku timu nyingine za Kundi D TP Mazembe na Mali Real Bamako zitakuwa na zikimenyana mjini Lubumbashi (DR Congo).