Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele amesema watahakikisha wanapambana ili kupata matokeo yatakayowapa alama tatu dhidi ya Singida Big Stars.

Young Africans itakuwa mgeni katika Uwanja wa CCM Liti mjini Singida baadae leo Alhamis (Mei 04), katika mchezo wa mzunguuko wa 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo ameweka wazi kuwa malengo yake ni kuona anaendelea kuifungia Young Africans mabao ya kutosha ili wazidi kujikita kileleni na kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu 2022/23.

“Malengo yetu ni kuendelea kuona tunapata ushindi katika kila mchezo ambao upo mbele yetu, tunatambua huu mchezo ni mgumu lakini lazima tupambane kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.”

“Kwangu binafsi ni kuona naendelea kuipambania Young Africans kwa kufunga mabao ya kutosha ili kufikia ndoto tulizojiwekea kama timu ambazo ni kutwaaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.” amesema Mayele

Mayele kwa sasa ndiye kinara wa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu Bara akiwa anayo 16 sawa na mabao aliyoyafunga msimu uliopita katika ligi hiyo akimaliza wa pili nyuma ya kinara George Mpole aliyekuwa Geita Gold FC.

Uboreshaji miundombinu bora TANICA waanza
Matumizi nishati safi: Mitungi 100,000 kutolewa bure