Mshambuliaji hatari wa Mabingwa wa Soka Tanzania Young Africans Bara Fiston Kalala Mayele, amewaomba Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa bila kukosa kesho Jumatano (Mei 10), ili kuipa nguvu timu yao.
Young Africans itakua mwenyeji wa mchezo wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kuanzia saa kumi jioni.
Mayele amesema kufika kwa wingi kwa Mashabiki na Wanachama Uwanja wa Benjamin Mkapa ni sehemu ya silaha ambayo itaiwezesha Young Africans kupata matokeo mazuri katika mchezo huo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho.
Amesema kuna kila sababu ya Mashabiki na Wanachama kuujaza Uwanja huo na kuwa sehemu ya historia ya klabu hiyo katika kipindi hiki ambacho wanasaka Rekodi ya kutinga Fainali ya Michuano ya CAF kwa mara ya kwanza.
“Itakuwa furaha kubwa kuona Young Africans wakicheza fainali na mimi nikiwa sehemu ya historia ya klabu hii, naamini tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu wa kesho pale kwa Mkapa, mashabiki waje kwa wingi, uwapo wao utatuzidishia hamasa na nitajitahidi kufunga ili tute- teme wote,” amesema Mayele.
Aidha, amesema anafahamu hautakuwa mchezo mwepesi na wapinzani wao watakuwa wamechukua muda kuwasoma kama ambavyo wao, Young Africans wanafanya.
“Hatua hii ni ya matokeo zaidi, ushindi pekee ndio utatuvusha kwenda mbele, wachezaji tunalitambua hili, tumejipanga na tunaendelea kujiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri hapa nyumbani kabla ya kwenda kurudiana nao kwao,” amesema Mayele
Mayele amesema kwake litakuwa jambo la kuumiza moyo kama watashindwa kupata ushindi kwenye mchezo huo wa kesho Jumatano utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Mashabiki siku zote ni mchezaji wa 12, kama wachezaji tunaomba waje kwa wingi kutupa sapoti na sisi hatutawaangusha, tunataka kucheza fainali ya michuano hii,” ameongezea Mayele.
Mayele kesho Jumatano (Mei 10) anategemewa kuongoza safu ya ushambulizi ya Young Africans kwenye mchezo huo wa mkondo wa kwanza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, utakaochezwa majira ya saa kumi jioni kabla ya kurudiana Mei 17 nchini Afrika Kusini.