Mshambuliaji hatari wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele ameendelea kutangaza hali ya hatari kwa timu za Tanzania msimu huu 2022/23.
Mshambuliaji huyo hadi sasa ameshafumania nyavu mara tatu katika michezo minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara aliyocheza akiwa na Young Africans, huku akitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani leo Jumatatu (Oktoba 03) dhidi Ruvu Shooting.
Mayele amesema dhamira yake ni kuisaidia Young Africa kutetea ubingwa kisha kufanikisha lengo la kuwa kinara wa kupachika mabao katika Ligi ya Tanzania Bara.
Amesema msimu huu wamejipanga kufanya mambo makubwa zaidi kwa kushirikiana ndani na nje ya Uwanja, hivyo atahakikisha anatumia nafasi hiyo kufikia malengo ya klabu na yake binafsi.
“Msimu uliopita haukuwa mbaya kwangu na kwa Young Africans kiujumla, ila kuna baadhi ya sehemu tuliteleza na kushindwa kufikia baadhi ya malengo binafsi na ya klabu kwa ujumla licha ya tulitimiza asilimia kubwa sana ya kile tulichokipanga,”
“Kama klabu tumejipanga kuendelea tulipoishia, ila binafsi natamani kufanya vizuri zaidi. Naamini Young Africans ya msimu huu ni bora sana, kuna kila aina ya mchezaji anayeweza kuibeba timu hivyo naamini kwa mchango mkubwa wa wenzangu nitafanya makubwa zaidi.”
“Kila mchezaji anatamani kuwa bora na kuchangia mafanikio ya timu kutokana na eneo lake analocheza. Kipa hataki kufungwa wala beki hataki kupitwa hivyo na mimi kama mshambuliaji natamani kufunga zaidi na ikiwezekana kuvunja na kuweka rekodi zilizopo kwenye ligi ya ndani na Kimataifa hivyo nipo tayari kuipambania Young Africans.” amesema Mayele
Mayele alianza msimu kwa kuifunga Simba SC mabao mawili katika mechi ya Ngao ya Jamii ambayo Young Africans ilishinda 2-1, kisha akafunga bao moja moja kwenye mechi za Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union na Mtibwa Sugar kabla ya kucheza michezo miwili ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini na kufunga hat-trick mbili kwa kila mechi.