Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Kalala Mayele amesema walikua na kila sababu ya kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, endapo wangepata ushindi mzuri Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Jumapili (Oktoba 08).
Katika mchezo huo, Young Africans ililazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Al Hilal, hali ambayo iliifanya klabu hiyo kuwa na wakati mgumu jana Jumapili (Oktoba 16) ilipocheza ugenini Khartoum-Sudan kwa kuambulia kichapo cha 1-0.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Mayele amesema ilitakiwa washinde mchezo wa nyumbani, ili kuufanya mchezo wa ugenini kuwa rahisi.
“Tulikosea sana kutoka sare hapa nyumbani, naamini hilo ndio lilituweka katika mazingira magumu tulipocheza ugenini dhidi ya Al Hilal, kama mambo yangekua mazuri hapa tungefanikiwa kuendelea na Michuano hii.” amesema Meyele
Young Africans imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, na jana ilifungwa 1-0 ugenini.