Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele amesema kuwa yeye pamoja na wachezaji wenzake ambao waliukosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika wakiwa na Klabu ya AS Vita wanatarajia kuupata msimu huu wakiwa na klabu ya Tanzania.
Mayele na wachezaji wengine ambao walicheza wote AS Vita kama Djuma Shabani, Yannick Bangala na Jesus Moloko waliukosa ubingwa wa Shirikisho mwaka 2018 ambapo walifungwa na Raja Casablanca katika fainali ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 6-1, fainali ya kwanza AS Vita 1-3 Raja na ya pili Raja 3-0 AS Vita.
Jumapili (Mei 28) Young Africans watacheza Mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha mchezo wa pili utapigwa Juni 3, nchini Algeria.
Mayele amesema: “Tulikosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho tukiwa na AS Vita ambapo tulifungwa dhidi ya Raja Casablanca jambo ambalo kwa kweli lilituumiza lakini kwa sasa tunayo nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa tulibeba kombe hili.
“Kupitia Young Africans tunakwenda kucheza fainali dhidi ya USM Algers niwaambie mashabiki wetu kuwa tunayo kiu kubwa ya kulibebe kombe hili na naamini tunakwenda kulibeba hili kombe kwa kuwa tunao uwezo mkubwa wa kufanya hivyo.”