Hasira ya Kufungwa na Kutolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Al Hilal ya Sudan, huenda ikawa Silaha itakayotumiwa na Wachezaji wa Young Africans kuiangamiza Simba SC Jumapili (Oktoba 28).
Miamba hiyo ya Soka la Bongo inakwenda kukutana Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikitoka kushiriki Michuano ya Kimataifa mwishoni mwa juma lililopita, ambapo Simba SC ilikutana na Primeiro de Agosto ya Angola.
Mshambuliaji hatari wa Young Africans Fiston Kalala Mayele amefichua siri ya kilichotokea baada ya mchezo dhidi ya Al Hilal ya Sudan na kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC.
Mayele amesema baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika walikutana Wachezaji wote na kufanya kikao chao wenyewe kuangalia wapi walipokosea na wanatakiwa kufanya nini kwenye mchezo ujao.
Amesema kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao hicho, anaamini kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza dhidi ya Simba SC Jumapili (Oktoba 23), atakuwa na ari kubwa ya kujituma zaidi ya ilivyokua kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal.
“Kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza kwenye mchezo unaofuata atakwenda kujituma zaidi ya ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita, kwani hiyo ni silaha kufanya vizuri kama malengo yetu yalivyo na tulivyokubaliana wenyewe ndani ya kikao chetu.”
“Jinsi gani tumejipanga kucheza dhidi ya Simba SC na mchezo utakuwaje, hayo yote yataongezewa nguvu katika maandalizi yetu, lakini tunajua tunakwenda kufanya nini siku hiyo.”
“Hakuna mchezo dhidi ya Simba SC uliowahi kuwa rahisi, ila lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunafanya vizuri, ndio maana tunasema waacheni waje tuwaonyeshe.” amesema Mayele
Mayele hajawahi kuifunga Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu tangu aliposajiliwa na Young Africans, zaidi ya kuiadhibu klabu hiyo ya Msimbazi katika Michezo ya Ngao ya Jamii, akifunga bao moja na la ushindi mwanzoni mwa msimu uliopita, huku akifanya hivyo tena mwanzoni mwa msimu huu kwa kufunga mabao mawili.