Bingwa wa zamani wa dunia wa masumbwi, Floyd Mayweather amempiga kikatili bingwa wa michezo ya ngumi na mateke, Tenshin Nasukawa katika pambano la maonesho lililomalizika muda mfupi uliopita nchini Japan.
Mayweather ambaye ameshiriki pambano hilo la maonesho lililokuwa na raundi tatu tu, amelimaliza ndani ya raundi moja na kujizolea pesa nyingi.
Mbabe huyo ambaye ameshastaafu mchezo wa masumbwi, aliingia ulingoni akiwa anacheka na kufanya utani mwingi kama mtu ambaye anaingia kwenye maonesho na sio pambano.
Hata hivyo, baada ya kengele ya kuanza pambano kusikika, Mayweather aligeuka chui na kumpiga ngumi mbaya usoni Nansukawa iliyompeleka chini.
Mbabe huyo wa Japan alifanikiwa kuamka baada ya kuhesabiwa na muamuzi, lakini aliporejea tu alipigwa tena na kurudi chini.
Ngumi ya mwisho ya Mayweather iliyompeleka Nasukawa chini kwa mara ya tatu ilisababisha timu ya mpiganaji huyo kuingilia kati na kurusha taulo ulingoni kuashiria kuomba kumalizika kwa pambano ili wamuokoe bondia wao.
Mpiganaji huyo wa Japan alionekana akiwa analia kwenye kona ya timu yake asiamini kilichotokea.
Nasukawa ambaye alikuwa na rekodi ya kutopoteza pambano lolote katika mchezo wa Kickboxing, aliahidi kuchukulia maonesho hayo kwa uzito wa juu na kwamba angempiga Mayweather kwa Knockout.
Hata hivyo, wataalam wa masumbwi duniani walikuwa wanalikosoa pambano hilo tangu awali wakieleza kuwa Nansukawa hatoshi kupambana na Mayweather hata kidogo.
Promota maarufu wa mapambano na Boss wa Top Rank Promotion, Bob Arum aliyekuwa anafanya kazi na Manny Pacquio alisisitiza kuwa pambano hilo lilikuwa maigizo na kwamba watakaoenda kuliangalia ni wendawazimu.
Mayweather amesisitiza kuwa bado amestaafu masumbwi na kwamba alichofanya ni maonesho tu na anarudi kwenye kiti chake cha ustaafu. Pambano hilo haliongezi rekodi yoyote kwenye historia ya mapigano ya wawili hao.
Baada ya pambano, Mayweather alimkabidhi Nasukawa tuzo aliyokuwa amekabidhiwa na kumtia moyo kuwa ni mpiganaji mzuri na anaweza.