Bondia asiyepigika, Floyd Mayweather amevuliwa mkanda wa ubingwa wa WBO, uzito wa Welterweight unaohusisha kilo 67 na 77 ambao alishinda mwezi Mei mwaka huu dhidi ya Manny Pacquiao kutokana na kushindwa kufuata sheria na kanuni za Shirikisho hilo.

Kamati ya mashindano ya WBO imesema kwamba haina jinsi ya kufanya zaidi ya kumvua mkanda huo Mayweather ambaye ameshindwa kulipa ada ya $200,000 kutoka kwenye pambano alilopigana na Pacquiao. Pambano lililokuwa na gharama kubwa zaidi katika historia ya masumbwi duniani.

Kwa mujibu wa shirikisho hilo, Ijumaa ilikuwa siku ya mwisho kwa Mayweather kutimiza vigezo vya ubingwa wa WBO ikiwemo kulipa ada hiyo inayochukuliwa kama sehemu ya chanzo cha mapato yanayoendesha shirikisho hilo.
Bondia Timoth Bradley Jr. anatarajiwa kupewa mkanda huo baada ya mwezi uliopita kumpiga kiutata, Jessie Vargas katika pambano la kutafuta bingwa wa muda wa uzito huo.

Hata hivyo, Mayweather mwenye umri wa miaka 38 amepewa siku 14 za kukata rufaa.

Mayweather bado anashikilia ubingwa wa welterweight na super-welterweight wa WBC na WBA, ingawa kwa mujibu wa sheria za mchezo huo, bondia haruhisiwi kushika ubingwa wa dunia kwa madaraja mbalimbali.

Udhalilishaji Wamnyima Ulaji Uwanjani
Al Shabaab yadai kuhusika na mauaji ya watu 14 Kenya