Imefahamika kuwa Uongozi wa Simba SC upo katika mazungumzo na makocha wawili, ili kufanikisha mpango wa kluziba nafasi ya Kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ aliyeondoka klabuni hapo Jumanne (Novemba 08).
Robertinho alisitishiwa mkataba wake Simba SC, baada ya kufikia makubaliano na Uongozi wa klabu hiyo, ikiwa ni siku mbili baada ya kikosi cha Mnyama kukubali kuchapwa bakora 5-1 na Young Africans.
Taarifa kutoka Simba SC zinadai kuwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa USM Alger ya Algeria, Abdelhak Benchikha na Kocha wa Viungo wa APR ya Rwanda, Adel Zrane raia wa Tunisia ndio wanapewa kipaumbele kwa sasa klabuni hapo.
Benchikha ambaye ni raia wa Algeria, anatajwa kuja kuchukuwa nafasi ya Robertinho Oliveira ‘Robertinho’ huku Zrane ambaye aliwahi kuwa sehemu ya Benchi la Ufundi la Simba SC akitarajiwa kurejea ndani ya klabu hiyo kuchukuwa nafasi ya Corneille Hategekimana.
Taarifa hizo zimesisitiza kuwa, wawili hao wapo katika mazungumzo na mapema ndani ya juma hili watakamilisha, hususan kocha wa viungo kabla ya kumalizika kwa mapumzuko ya Kalenda ya FIFA.
Mtoa taarifa hizi amesema katika meza ya Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, imepokea majina ya makocha wengi akiwamo Sven Vandenbroeck na Benchikha, ambaye jina lake limepita na kuanza mchakato wa mazungumzo naye mapema.
“Tunahitaji kufanya haraka mchakato wa kupata kocha mkuu na wa viungo, hao (Benchikha na Zrane) wamekuwa katika chaguo na mazungumzo yakienda vizuri kwa pande Zote mbili wakikubaliana watakuwa sehemu yetu ya benchi la ufundi.”
“Tunahitaji kufanya mchakato huo mapema ili timu inapokwenda katika nashindano ya kimataifa, mchezo wetu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Asec Mimosas tuwe tumeshampata Kocha Mkuu,” alisema mtoa habari huyo.
Alipotafutwa Meneja wa ldara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally kuhusu mchakato wa kupatikana kwa Kocha Mkuu na Kocha wa viungo, amesema uongozi upo katika mchakato huo na wakati wowote kuanzia kesho Jumanne (Nobemba 14) wanaweza kumtangaza kocha Mkuu ambaye atakuja kuchukuwa mikoba ya Robertinho.