Uongozi wa Young Africans unahaha kumpata mbadala wa kiungo mkabaji kutoka nchini Uganda Khalidi Aucho, ambaye kwa sasa ni tegemeo katika kikosi cha Kocha Mkuu Miguel Gamondi.

Hiyo ni katika kuelekea usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa kwaka huu ambalo Young Africans wamepanga kukifanyia maboresho kikosi chao ili kifanye vema katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Nafasi hiyo pia inachezwa na viungo wazawa Jonas Mkude na Zawadi Mauya ambao wameonekana kushindwa kuonyesha ushindani mbele ya Aucho.

Kwa mujibu wa mmoja wa Mabosi kutoka ndani ya Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, amesema kuwa viongozi wa timu hiyo, wanahaha kumpata mbadala wa Aucho atakayesajiliwa katika dirisha dogo.

Bosi huyo amesema kuwa wapo katika jitiahada za kumpata kiungo mkabaji wa kigeni, mwenye uwezo wa kuchezesha timu, kukaba na kuanzisha mashambulizi katika goli la wapinzani.

Ameongeza kuwa kikubwa Benchi la Ufundi la timu hiyo, linaloongozwa na Gamondi limekabidhi ripoti ya kiungo mkabaji anayezuia mashambulizi kuanzia juu kabla ya kufika kwa mabeki wao wa kati.

“Kwa asilimia kubwa tayari tumekamilisha usajili wa wachezaji ambao wapo katika mipango yetu, katika usajili unaokuja wa dirisha dogo, kwa kufuata ripoti ya kocha wetu Gamondi.

“Nafasi hizo ni winga, mshambuliaji ambazo tayari wapo wachezaji tuliomalizana kilichobakia ni kutangazwa pekee, lakini bado nafasi ya kiungo mkabaji ambayo inatupa ugumu katika kumpata ambaye anakuja kuwa mbadala wa Aucho.

“Tunataka kiungo mkabaji aina ya Aucho ambaye anawazuia wapinzani kuanzia juu, kabla ya kuwafikia mabeki wa kati ambaye ana uwezo wa kutuliza mashambulizi,” amesema bosi huyo.

Rais wa Young Africans Hersi Said hivi karibuni alisema kuwa: “Tumeshamalizana na baadhi ya wachezaji waliokuwepo katika mipango yetu katika dirisha dogo, kilichobakia ni kutangazwa pekee.”

Man City, Liverpool kuivurugia Arsenal
Chelsea kujibana usajili dirisha dogo 2024