Mkuu wa Benchi la Ufundi la Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ameutaka Uongozi wa klabu hiyo kuanza mchakato wa kumsaka Mshambuliaji hatari zaidi ya Jean Baleke na kiungo atakayekuwa mbadala wa Clatous Chama.
Kauli hiyo ameitoa mara baada ya timu hiyo, kutolewa na Wydad AC ya Morocco kwa mikwaju wa Penati katika mchezo Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika uliopigwa Ijumaa (Aprili 28) mjini Casablanca.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa mara baada ya mchezo huo, haraka kocha huyo alifanya kikao na baadhi ya Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, waliosafiri na kikosi hicho.
Ally amesema kuwa anaamini ubora wa wachezaji lakini, maboresho makubwa yanahitaji katika kuelekea usajili wa msimu ujao, ameomba asajiliwe mshambuliaji mwenye uwezo zaidi ya Baleke.
Amesema kuwa kocha huyo anapata ugumu wa kupata matokeo kimbinu, kutokana na kuwepo mshambuliaji mmoja pekee tishio kwa wapinzani ambaye ni Baleke pekee.
Ameongeza kuwa pia kocha huyo katika kikao hicho ametoa mapendekezo ya kusajiliwa kiungo mshambuliaji mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao kwa wenzake zaidi ya Chama.
“Baada ya mchezo wa marudiano dhidi ya Wydad AC, kocha Robertionho alifanya kikao na viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi tukiwa hotelini Morocco.”
“Kikubwa ni kutoa tathimini ya timu hiyo, katika ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika na katika kikao hicho ametoa mapendekezo ya usajili wa wachezaji wapya.”
“Lengo ni kutengeneza kikosi bora na tishio katika Ukanda huu wa Afrika na zaidi kufika hatua ya Nusu Fainali hadi Fainali katika michuano ya Kimataifa.” Amesema Ahme lly