Uongozi wa Tanzania Prisons umesema baada ya kumpata kocha mkuu atakayekuja kukinoa kikosi cha timu hiyo, wataweka kambi visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2023/24 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Tanzania Prisons, Enock Manguku, amesema baada ya kuondoka kwa Kocha wao, Abdallah Mohamed ‘Bares’, wamelazimika kuendelea kusalia ndani ya kambi yao jijini Mbeya hadi hapo watakapokamilisha kumpata mrithi wake.
Amesema mipango yao ni kuweka kambi visiwani Zanzibar au jijini Dar es salaam baada ya kukamilisha zoezi zima la usajili.
Manguku amesema kwa sasa timu imeanza kambi jijini Mbeya kwa muda wa siku kadhaa na leo wanatarajia kumtambulisha kocha mpya tayari kwa kukiongoza kikosi chao kuelekea msimu ujao.
“Tumejipanga vizuri kuanzia usajili na tayari baadhi ya wachezaji wetu wameanza kuingia kambini na muda wowote kuanzia leo tutaweka wazi majina ya wachezaji tuliowasajili pamoja na kocha wetu mkuu,” amesema Manguku.
Ameongeza kuwa wako kwenye hatua ya mwisho ya mazungumzo na kocha huyo ambaye anakinoa kikosi cha timu hiyo kwa kutorudia makosa yaliyofanyika msimu uliopita ambayo yalisababisha kumaliza ligi kwa presha.
“Kila msimu ligi inakuwa na ushindani mkubwa, ukiangalia tumemaliza ligi tukiwa na presha kubwa ya kujinusuru kushuka daraja, jambo hilo hatuhitaji lijirudie katika msimu mpya, hivyo tutafanya usajili mzuri na kuimarisha benchi letu la ufundi,”amesema Manguku.