Klabu ya Simba SC inahusishwa na mpango wa kumsajili Beki kutoka nchini DR Congo na Klabu ya Cape Town City ya Afrika Kusini, Nathan Idumba Fasika.
Idumba alijunga na Cape Town City Julai 16, 2021 akitokea FC Saint Eloi ya kwao DR Congo, ambapo mkataba wake na Cape Town unatarajiwa kufikia kikomo Juni 30, 2026.
Hivi karibuni, Kocha wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliweka wazi kuwa safu yake ya ulinzi imekuwa na makosa mengi kuanzia michuano ya ndani hadi ya ile kimataifa.
Kwa sasa safu hiyo inayoongozwa na Joash Onyango pamoja na Henock Inonga imetengeneza Penati tatu zote zikitengenezwa na Onyango kwenye harakati za kuokoa hatari katika michuano ya kimataifa msimu huu.
Kutokana na hilo, chanzo kutoka Simba SC kimeeleza kuwa kutokana na Kocha wao raia Brazil, Robertinho kuendelea kusisitiza kuongeza beki wa kati, wanatarajia sasa kumalizana na Idumba ili kupunguza presha kwenye eneo hilo.
“Tunalazimika tena kutafuta beki mwingine atakayekuja kuongeza nguvu kikosini, jambo ambalo linatufanya kurejea mezani kuzungumza na uongozi wa Cape Town ili tumpate Idumba.”
“Nadhani unakumbuka mwanzo tulizungumza naye pamoja na timu yake ila dau likawa kubwa tukaamua kumsajili Mohamed Ouattara ambaye kocha bado haridhishwi naye jambo ambalo linatufanya tuingie sokoni tena kupata hitaji la kocha,” kimesema chanzo hicho.
Hata hivyo alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema: “Tumepanga kufanya usajili mkubwa kwa ajili ya msimu ujao, zaidi tutaangalia wale wachezaji ambao wanacheza mara kwa mara na sio wale wa historia, hivyo dirisha likifunguliwa hayo ndiyo malengo ila kwa sasa bado hatujaingia rasmi kwenye usajili.”