Hatma ya klabu za Mbao FC na Mbeya City kuendelea kuwa miongoni mwa klabu za Ligi Kuu msimu wa 2020/21, itafahamika leo jioni baada ya michezo ya mkondo wa pili ngazi ya mchujo kwenye viwanja vyao vya nyumbani.
Mbao FC watapambana kwenye uwanja wao wa nyumbani, CCM Kirumba mjini Mwanza wakiikaribisha Ihefu FC kutoka Mbeya kwenye mtanange ambao utakuwa unaangaliwa zaidi na mashabiki wengi wa soka nchini.
Mbeya City watakuwa mwenyeji wa Geita Gold kutoka mkoani Mwanza, kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Jumatano Julai 29 kwenye michezo ya mkondo wa kwanza, Mbao FC walibamizwa mabao 2-0 dhidi ya Ihefu FC kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbalizi, Mbarali mkoani Mbeya.
Kwa matokeo hayo, Mbao FC wana kazi kubwa ya kufanya, kupata ushindi wa kuanzia mabao matatu kwa sifuri na kuendelea ili kuwa na uhakika wa kuendelea kubaki Ligi Kuu msimu ujao, vinginevyo msimu ujao watacheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
“Wao walishinda kwao na sisi tunawakaribisha kwetu Mwanza, haitokuwa mechi rahisi kwao, tutawapa wakati mgumu sana,” alisema Waziri Junior, kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa amemaliza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheka na nyavu mara 13.
Kocha Mkuu wa Ihefu, Maka Malwisi alisema amejiandaa kikamilifu na mechi ya marudiano na anajua itakuwa ngumu, lakini amewaandaa vijana wake kukabiliana na kila hali.
“Nimeshawandaa vijana wangu kucheza mechi zote mbili, kwa hiyo najua ni jinsi gani na mfumo gani tutacheza,” alisema kocha huyo.
Timu ya Mbeya City wenyewe watalazimika kupata ushindi wa aina yoyote ile ili kubaki Ligi Kuu kwani katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Sekondari ya Nyankungu mjini Geita Julai 29, walilazimishwa sare ya bao moja kwa moja wakiwa ugenini.
Ihefu FC ilishika nafasi ya pili kwenye Kundi A, huku Geita nayo ikimaliza katika nafasi kama hiyo kwa upande wa Kundi B, wakati Mbeya City, ikishika nafasi ya 15 na Mbao FC ya 16 kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo timu zitakazopata matokeo ya jumla zitaungana na zingine 16 kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.