Klabu ya Mbao FC inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara, imesaini mkataba wa udhamini wa mwaka mmoja na kampuni ya uagizaji wa magari ya mizigo GF Trucks & Equpments wenye thamani ya shilingi milioni 140.
Akizungumza na wanahabari kwenye ukumbi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), afisa masoko wa kampuni hiyo, Kulwa Bundala alisema ndani ya mkataba huo wataipatia klabu hiyo basi lenye thamani ya shilingi milioni 70 pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 70.
Upande wa Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Zephania Njashi ameishukuru Kampuni ya GF kwa kuingia nao mkataba huo na basi hilo litawasaidia katika safari mbalimbali kipindi hiki cha ligi kuu ya Tanzania bara.
Huo unakuwa udhamini wa pili kwa washindi hao wa pili wa Azam Sports Federation Cup, baada ya mwaka jana kupata udhamini wa Hawaii Products Supplies, watengenezaji wa maziwa ya Cowbell wenye thamani ya shilingi milioni 50 kwa msimu.