Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain Kylian Mbappe ameweka wazi kwamba hana mpango wa kuondoka klabuni hapo mwisho wa msimu huu licha ya kuhusishwa na Real Madrid.

Mbappe alijibu swali na waandishi wa habari alipoulizwa kama ana mipango ya kuondoka PSG na Mshambuliaji huyo alipinga.

“Hatua inayofuata ni kubeba ubingwa wa Ligi Mabingwa Ulaya, tulishafika fainali, Robo Fainali, nusu fainali, hadi raundi ya 16 bora, nimefanya kila jitihada tushinde, ubingwa tu ndio nataka kwa sasa, kuhusu wapi nitacheza? Basi ni Paris pekee, mimi ni mchezaji halali wa PSG,” amesema Mbappe.

Taarifa ziliripoti mwaka huu Mbappe alizinguana na wachezaji wenzake kwenye chumba cha kubadilishia nguo, kwa kile kilichodaiwa staa huyo anataka kujiona mkubwa zaidi ya klabu.

Kitendo hicho kiliwakera wachezaji wenzake kwa mujibu wa ripoti, lakini Mbappe alikana taarifa hizo akidai kila kitu kipo freshi tu.

PSG iliondolewa kwenye 16-bora ya Ligi Mabingwa Ulaya msimu huu na kwa mujibu taarifa klabu hiyo itaachana na kocha wake, Christophe Galtier, baada ya kuboronga.

Wakati huo huo, Lionel Messi na Neymar inasemakana huenda wakatimika mwisho wa msimu huu, lakini uamuzi kuhusu hatima ya Mbappe utabaki mikononi mwa klabu.

Mbappe bado anahusishwa na Madrid tangu walipomkosa katika dirisha la usajili kiangazi baada ya kuipotezea ofa iliyotolewa na klabu hiyo. Fowadi huyo atarejea dimbani kesho kukiwasha dhidi ya Lens kwenye mechi ya Ligue 1.

Waziri Mkuu atoa wito vita mmomonyoko wa maadili
Utoaji fedha za mikopo kwa makundi maalum wasitishwa