Klabu ya Paris St-Germain imelaumiwa kwa unyanyasaji wa kimaadili baada ya kumuacha Kylian Mbappe katika ziara ya maandalizi Asia huku Umoja wa Wanasoka wa Ufaransa ukisema kuwa utachukua hatua za kisheria.
Mfungaji huyo wa PSG anayeongoza kwa mabao kwa muda wote aliiambia klabu hiyo kuwa hataongeza mkataba, ambao umebaki miezi 12 tu.
Klabu inataka kumuuza Mbappe, mwenye umri wa miaka 24, sasa ipate ada, lakini Mbappe anapanga kubaki hadi mwishoni mwa mkataba wake.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliigharimu PSG kiasi cha Pauni milioni 165.7 kufuatia kuhamia kutoka Monaco mwaka 2017.
Baada ya Mbappe kuachwa katika kikosi cha PSG kilichoenda Japan na Korea Kusini, Umoja wa Wachezaji wa Kulipwa ulitoa taarifa: Mchezaji huyo anatakiwa naye kufurahia hali bora ya kazi kama wengine.