Mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe anataka kutatua ishu yake na mabosi wa klabu baada ya mvutano wa muda mrefu kuhusu mkataba.
Mbappe aligoma kusaini mkataba miezi kadhaa iliyopita, lakini sasa anataka kusahau yote yaliyotokea kati yake na mabosi na yupo tayari kujituma kwa ajili ya PSG.
Taarifa zinaeleza kuwa, Mbappe atasaini mkataba mpya na PSG utakaodumu hadi 2026, na endapo atafanya uamuzi huo atazima kelele za hatma yake ndani ya klabu hiyo.
Mkataba wake utajumuisha kipengele kipya kwa ajili ya dirisha la usajili la majira ya kiangazi msimu ujao na kitamwezesha kusajiliwa na Real Madrid.
Mbappe alikuwa mgumu kuweka wazi kuwa anatamani kujiunga na Madrid siku za usoni, lakini PSG iligoma kumuacha aondoke huru mwakani, ndio maana ishu ya mkataba ikaletwa tena.
Mchezaji huyo aliondolewa katika kikosi cha kwanza cha PSG hadi atakapoweka mambo sawa na mabosi wa kabla ya kurudishwa.
Kabla ya kurejea kikosini Mfaransa huyo alikuwa akifanya mazoezi pekee yake. Tangu aliporejea katika kikosi cha PSG kinachonolewa na Luis Enrique, Mbappe ameshatupia kambani mabao matatu katika mechi mbili za Ligue l alizocheza msimu huu.
Kesho Jumapili (Septemba 03), mchezaji huyo ataiongoza PSG katika mchezo wa mwisho dhidi ya Lyon kabla ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa.
Miamba hiyo ipo katika nafasi ya nane baada ya kuanza vibaya msimu. Katika michezo mitatu PSG imeshinda mmoja.