Mshambuliaji Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe amewajia juu Mashabiki wan chi hiyo kutokana na kutoonesha heshima kwa Lionel Messi katika misimu yake miwili ya Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1.
Messi alijiunga na mabingwa hao wa Ufaransa mwaka 2021 kwa uhamisho wa bure kutoka FC Barcelona na licha ya kushinda ligi mara mbili, Mshambuliaji huyo alitatizika kuzoea maisha ya PSG.
Messi mwenye umri wa miaka 35, alizomewa na kukejeliwa na mashabiki wa PSG kufuatia timu hiyo kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu miwili mfululizo.
Messi aliamua kutoongeza mkataba wake na PSG mwishoni mwa msimu huu na atajiunga na Inter Miami ya Ligi Kuu ya Marekani.
“Tunazungumza kuhusu uwezekano wa mchezaji bora katika historia ya soka,” alisema Mbappe akiliambia jarida la Italia Gazzetta dello Sport.
Mbappe alimtetea mchezaji mwenzake wa zamani wa klabu hiyo na kusema alistahili heshima zaidi
“Sio habari njema wakati mtu kama Messi anaondoka. Binafsi sijaelewa kwa nini watu wengi walifarijika kuondoka. Tunazungumza kuhusu Messi, anapaswa kuheshimiwa lakini badala yake, hakupata heshima aliyostahili Ufaransa. Ni aibu, lakini ndivyo ilivyokuwa.”
Mbappe pia aliongeza kuwa hakuwahi kuiomba PSG kumruhusu kuhamia Real Madrid msimu huu wa joto, akithibitisha kwamba ana furaha kucheza katika mji mkuu wa Ufaransa msimu huo, lakini hataongeza mkataba wake na klabu hiyo.
Mbappe alizua taharuki alipotuma barua kwa klabu hiyo ikieleza kuwa hana nia ya kuongeza mkataba wake na PSG ambao unamalizika mwaka 2024.
PSG wana hatari ya kumpoteza Mbappe bila malipo Juni 2024. Pia atakuwa huru kusaini mkataba wa awali wa mkataba na klabu mpya kuanzia Januari iwapo ataamua kuona mwaka uliosalia wa mkataba wake na PSG.
“Sikuomba kuuzwa au kwenda Real Madrid,” alisema Mbappe.
“Nimethibitisha kuwa sitaki kuamsha mwaka wa ziada uliotarajiwa katika mkataba. Hatujawahi kuzungumza kuhusu kuongezwa upya na PSG, lakini nina furaha kubaki hapa msimu ujao.”
Madrid waliwahi kumtaka Mbappe mwenye umri wa miaka 24, siku za nyuma lakini wakashindwa kumpata. Alitia saini mkataba wa nyongeza na PSG Mei mwaka jana.
Hata hivyo, klabu hiyo ya Hispania inaijenga upya timu yao baada ya kumpoteza mshindi wa Ballon d’Or Karim Benzema na huenda wakaelekeza macho yao kwa Mbappe, ambaye amemaliza kama mfungaji bora wa Ligue 1 kwa misimu mitano iliyopita.