Mshambuliaji wa Mabingwa Wa Kombe La Shirikisho Tanzania bara (ASFC) Azam FC Mbaraka Yusuph amekuwa sehemu ya wachezaji wa klabu hiyo walioanza mazoezi jana Jumatano Uwanja wa Azam complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Mbaraka alirejea mazoezini kwa mara ya kwanza, baada ya kuwa nje kwa msimu mmoja akifanyiwa matibabu, ambapo alipelekwa Afrika Kusini kufanyiwa matibabu na akarejea nchini bila kujihusisha na michezo yoyote zaidi ya kujifua mwenyewe ili kujiweka fiti zaidi.
Mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kutamba na Kagera Sugar kabla ya kutua Azam FC, amesema amesema kwa sasa yupo fiti kwa asilimia mia moja, na anatarajia kuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC, pindi ligi itakaporejea kuanzia Juni Mosi.
“Nilikuwa nimepona tangu msimu unaanza lakini daktari aliniambia kuwa sipaswi kucheza mpira wa ushindani zaidi ya kujiweka vizuri mwenyewe hivi sasa nimepona na mashabiki wategemee kuniona uwanjani tutakapoanza michezo ya ligi na kombe la shirikisho.”
“Suala la mimi kupata nafasi, nafahamu dawa yake ni kufanya vyema katika mazoezi na kuonesha kile ambacho ninacho, ninajua Azam FC ina washambuliaji wengi lakini kila mtu ana kitu Chake.” Amesema Mbaraka Yusuph.
Kikosi cha Azam FC, kimeanza mazoezi rasmi jana ikiwa ni siku chache baada ya kuruhusiwa kuendelea kwa shughuli mbalimbali za kimichezo nchini ili kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara, inayotarajiwa kuendelea mwezi ujao, Juni, 2020.
Katika mazoezi hayo, wachezaji wa Azam FC walionekana kupeana nafasi ikiwa ni sehemu ya tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona licha ya kuwa hadi sasa hakuna Lisa chochote kwa wachezaji wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara.