Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ameeleza kuwepo njama za kutaka kuchukua uhai wake na kutishiwa maisha.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mbatia ameeleza kuwa zipo njama zinazosukwa na watu wasiomtakia mema kwa lengo la kumuua. Alisema kuwa njama ya kwanza ni kutaka kumteka wakati anaelekea nyumbani kwake au mahala pengine na kisha kummaliza.

Mbatia alieleza kuwa njama nyingine ni kutaka kuwatumia vijana kwa kuwavalisha mavazi ya Chadema kisha wamshambulie kwa lengo la kumuua ili ionekana kuwa kulikuwa na mgogoro ndani ya Ukawa na amefanyiwa kitendo hicho na vijana wenye hasira juu ya mwenendo wa umoja huo.

Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, alitoa taarifa katika jeshi la polisi na kufungua jalada lenye kumbukumbu namba KW/RB/9600/2015.

Aidha, Mbatia alimrushia tuhuma Mwenyekiti Mwenza wa chama hicho, Bi. Leticia Mosore kuhusika katika njama kwa kushirikiana na  chama kingine cha siasa.

Alidai kuwa Bi. Leticia alipanga pia njama za kutaka kukihujumu chama kuratibu mpango wa kuwakusanya baadhi ya wenyeviti wa chama hicho kutoka mikoani ili wafike makao makuu ya chama hicho kwa pamoja ili wamfukuze Mwenyekiti huyo kwa madai kuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa Mbatia, njama hizo zilipangwa Septemba 19 mwaka huu ambapo baadhi ya wenyeviti wa chama hicho akiwemo mwenyekiti wa wa Makamishna wa chama hicho, Peter Mushenyela, walitumiwa fedha na makamo mwenyekiti huyo ili kufanikisha zoezi hilo.

Alisema mbali na wenyeviti hao, pia alituma fedha kwa wajumbe wengine wa mikoani ili waweze kushawishika kumuunga mkono katika njama zake hizo.

Hata hivyo, Mbatia anaeleza kuwa Mwenyekiti wa Makamishna wa chama hicho, Peter Mushenyena hakukubaliana na ushawishi wa Bi. Leticia na akamueleza Mbatia ambapo waliamua kuweka mtego.

“Baada ya kupata taarifa zile kutoka kwa Mwenyekiti wa Makamishna kwamba makamu mwenyekiti anapanga njama za kunidhuru, nilimuelekeza namna ya kuweka mtego,” alisema Mbatia.

Mbatia alieleza kuwa wajumbe mbalimbali waliletwa Dar es Salaam kutoka mikoani na kupangiwa katika hoteli moja kwa lengo la kujipanga kutekeleza tukio hilo.

Mushenyena alieleza kuwa walipewa posh ya kujikimu ya 60,000 kila siku na kuahidiwa kupewa shilingi milioni 10 kila mmoja endapo wangetekeleza agizo la kusoma hadharani waraka ambao wangekabidhiwa na Bi. Leticia ulioandikwa na watu wa chama kingine. Lengo likiwa kumchafua Mbatia, Lowassa  na viongozi wengine wa Ukawa.

Mbatia anaeleza kuwa anao ushahidi wa sauti, picha za mnato pamoja na video zinazoonesha kikao na njama zilizokuwa zinapangwa na Bi. Leticia na watu hao ambazo alidai kuwa ataziwasilisha mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura alithibitisha kupokea nyaraka za malalakimiko ya Mbatia.

Hata hivyo, Bi. Leticia alikanusha vikali tuhuma hizo na kudai kuwa tangu alipofanya mkutano na waandishi wa habari Septemba 17, hajawahi kufanya kikao chochote na hahusiki na njama yoyote dhidi ya Mbatia.

Bi. Leticia pia alidai kuwa bado hajapata taarifa rasmi kuhusu kufukuzwa au kusimamishwa uanachama kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Chama hicho, James Mbatia.

 

Nyosso Adai Kufanyiwa Hujuma
Mourinho Anusurika Na Adhabu Ya FA