Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia amezungumza kwa niaba ya Ukawa, kuhusu tuhuma zilizotolewa jana na Dk. Wilbroad Slaa dhidi ya Edward Lowassa na Chadema.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mbatia amesema kuwa Dk. Slaa aliudanganya umma kwa kukataa kuwa hakutangaza nia ya kugombea urais kupitia Ukawa kwa kuwa walikaa pamoja na yeye akasema ni bora zaidi.

“Wagombea wetu wa urais walikaa pamoja, na Dk. Slaa alisema wazi kuwa yeye ni bora zaidi ya wote, sasa leo anasema hakuwahi kutia nia,kweli?,” alihoji.

Alidai kuwa Dk. Slaa aliudanganya umma kwa kusema yeye ni msafi huku akidai kuwa alikataa rushwa ya shilingi milioni 500 mwaka 2007 na hakuwahi kusema suala hilo hadi jana alipokuwa akimzungumzia Edward Lowassa.

“Eti suala la rushwa zaidi ya miaka 7 usiripoti halafu uje useme leo, kusema uongo ni kazi sana,” alisema Mbatia.

Aidha, alimkosoa Dk. Slaa kwa kuwahusisha maaskofu na vita ya kisiasa inayoendelea huku akiwaomba radhi watumishi hao wa dini kwa kile kilichosemwa dhidi yao akidai kuwa ni vyema angeacha wanasiasa wasuguane wenyewe bila kuwasisha viongozi wa dini.

Mbatia meeleza kuwa tukio hilo ni mfululizo wa matukio yanayofanywa na CCM katika kutafuta namna ya kuiyumbisha Ukawa na kuitoa kwenye reli ili iache hoja za msingi za kampeni na kuanza kumjibu mtu mmoja mmoja.

“Hivi ni ashiria kwamba CCM wameshindwa hoja, mara kuleta mambo ya udini, mara wanaibua hili mara lile. wanataka kuchafua amani yetu kwa kuigiza masuala ya dini.”

Katika hatua nyingine, mbatia amewataka wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM, Samuel Sitta na Harison Mwakyembe wanaotafuta kufanya mdahalo na Lowassa kumuacha apumzike kwa kuwa mgombea huyo wa urais sio saizi yao na kwamba kama wanataka mdahalo wamualike yeye.

Mbatia pia alihoji sababu za Dk. Slaa kumvaa Frederick Sumaye wakati hoja yake ilikuwa ni Edward Lowassa na sio mtu mwingine kama alivyodai.

“Tukisema tuibue masuala yote na kashifa za kuuzwa kwa nyumba, kuna mtu atabaki salama?” Alihoji.

Aliwataka watanzania kuendelea kushikamana kuhakikisha wanakamilisha nia yao ya kuipata katiba mpya ambayo hivi sasa inaongozwa na Edward Lowassa.

Zitto Kabwe: Tutamsaidia Dk. Slaa, Tutamaliza
Mabango Ya Wagombea Marufuku Vituo Vya Mabasi Dar