Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ametoa msimamo wa chama chake kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na vyama vya upinzani wakati ambapo chama hicho kinapanga kumpata mgombea mmoja wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu, Octoba mwaka huu.

Akiongea na Radio One hivi karibuni, Mbatia alikanusha tetesi kuwa viongozi wa umoja huo wameshindwa kuelewana katika kumpata mgombea mmoja watakayemsimamisha kuwania kiti cha urais, tetesi zilizomnyoshea kidole mwenyekiti huyo kuwa kati ya wanaopinga utaratibu unaoendelea.

“UKAWA ipo leo, UKAWA iko kesho, UKAWA ipo tarehe Octoba tarehe ya uchaguzi hadi Tanzania ipate katiba hai,” alisema mwenyekiti huyo wa NCCR Mageuzi.
ukawa

Alibainisha kuwa chama chake kitaendelea kushirikiana na viongozi wengine wa vyama vya upinzani wanaounda umoja huo huku akiwataka viongozi hao kuweka mbele nia ya umoja huo na maslahi ya watanzania katika kuelekea uchaguzi mkuu na kupata katiba mpya.

“UKAWA ni Umoja wa Katiba ya Wananchi, hakuna mtu mwenye hati mil
iki ya UKAWA. UKAWA ni chombo cha watanzania, naomba wenzangu tushirikiane na tuache ubinafsi,”alisema.

Taarifa zinaeleza kuwa UKAWA wanatarajia kumsimamisha mgombea mmoja wa kiti cha urais baada ya Chama Cha Mapinduzi kumaliza mchakato na kumtangaza mgombea wao.

Hata hivyo, tayari baadhi ya viongozi wa UKAWA wametangaza nia ya kuwania urais akiwemo Prof. Ibrahim Lipumba wa chama cha wananchi (CUF).

Cannavaro: Wachezaji Tunaumia Kuliko Mashabiki Wa Soka La Bongo
Luis Nani Kucheza Soka Uturuki