Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema kuwa sio sahihi Spika Ndugai kushambuliwa kutokana na hoja yake bali hoja hiyo ichukuliwe na kujadiliwa kwa mtazamo chanya.
Mbatia amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari Ilala jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za kufunga mwaka 2021 na kufungua mwaka 2022 ambapo amesema mihimili ya Bunge na Serikali ikisigana ndiyo afya katika Taifa.
Itakumbukwa Desemba 28 mwaka huu, akiwa Jijini Dodoma katika mkutano wa pili wa wanakikundi cha Mkalile Ye Wanyusi Spika Ndugai alitetea uamuzi wa Bunge wa kuanzisha na kupitisha tozo za miamala ya simu kuliko kuendelea kukopa.
Lakini pia katika utiaji wa saini wa mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR uliofanyika Ikulu Dar es Salaam, Rais Samia alisema Serikali itaendelea kukopa ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo kwa awamu nyingine.
Mbatia amesema mambo haya ni kwa maslahi ya taifa hivyo hakuna haja ya kuweka usiri.
“Haya mambo sio chama kimoja wala mambo ya jikoni, wengine wanasema Ndugai alitakiwa akamnong’oneze Rais Samia. Je akifanya hivyo nani atalipa hilo deni? Haya ni mambo ya maslahi ya umma” amesema Mbatia.
“Migongano ya Bunge na Serikali ni afya kwa Taifa, mahali penye mawazo kinzani yanachangia Taifa kustawi. Ndugai ametoa hoja kuhusu suala la kukopa na ameonyesha taifa liko wapi katika mchakato huu sasa ni kweli? Amesema Mbatia.
“Ndugai wanamtukana tu na kumshambulia tu, lakini ametuamsha kutoka usingizi kwa kusema ukweli,” amesema Mbatia
“Tusimtukane Ndugai bali tuchukue hoja na kuijadili kwa mtazamano chanya. Mawazo kinzani yenye ukweli yajadiliwe kwa mtazamo chanya. Spika Ndugai amefunguka kuzungumza ukweli hadharani, ” amesema Mbatia.