Uongozi wa klabu ya Mbeya Kwanza FC umetangaza ZAWADI NONO kwa wachezaji wao endapo watafanikiwa kuibanjua Young Africans katika mchezo wa mzunguuko wa saba wa Ligi kuu Tanzania Bara.
Mbeya Kwanza FC inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Young Africans siku ya Jumanne (Novemba 30) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.
Mwenyekiti wa klabu hiyo inayoshiriki kwa mara ya Kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22 Mohamed Mashango amesema, wametangaza ZAWADI NONO kwa wachezaji wao lakini bado hawajaiweka wazi.
Amesema zawadi hiyo ipo na imeshaandaliwa kwa ajili ya wachezaji endapo wataifunga Young Africans kwenye mchezo huo, lakini wanahofia kuiweka wazi kwa sasababu wanahisi huenda ikawatoa mchezoni wachezaji wao.
“Hatutaki kutangaza ni zawadi gani tutatoa kwa wachezaji wetu, lakini ukweli ni kwamba tumeshaiandaa, itatoka tu endapo lengo litatimizwa na wapambanaji wetu.”
“Suala la kuiweka wazi zawadi hiyo mapema, tunahofia huenda likawatoa mchezoni wachezaji wetu na wakajikuta wanapaniki kabkla ya siku ya mchezo.” amesema Mohamed Mashango
Mbeya Kwanza FC ilipoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu mwishoni mwa juma lililopita, kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons waliokua nyumbani Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.