Wakati klabu ya Young Africans ikiendelea kuhusishwa na mpango wa kumsajili Mshambuliaji wa Mbeya Kwanza FC Chrispin Ngushi, Uongozi wa klabu hiyo Kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati umeombwa kufuata utaratibu.

Young Africans imejizatiti kufanya usajili wa baadhi ya wachezaji katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo, ili kuboresha makali ya kikosi chao na kufikia lengo la kurejesha heshima ya Ubingwa wa Tanzania bara unaoshikiliwa na Simba SC kwa misimu minne mfululizo.

Mwenyekiti wa Mbeya Kwanza FC Mohammed Mashango amesema taarifa za Chrispin Ngushi, kuwaniwa na Young Africans wanazisikia katika vyombo vya habari na kuziona kwenye mitandao ya kijamii, lakini hakuna utaratibu wowote uliofuatwa hadi sasa.

Amesema endapo Young Africans wana dhamira ya kumsajili Mshambuliaji huyo, wanapaswa kufuata utaratibu na ikitokea wanafikia muafaka watamuachia Ngushi.

“Hadi sasa bado hatujapata ofa yoyote kutoka kwa Young Africans lakini tumekua tukisikia kuwa wanamuhitaji lakini bado hawajafika kwetu kama wakija tukafanya mazungumzo na tukafikia makubaliano mazuri basi kila kitu kitakuwa wazi.

“Sisi kama timu tupo tayari kumuachia Chrispin kwenda Young Africans kwani lengo letu ni kuona vijana wetu wanakuza vipaji, kwa hiyo hatutakuwa na pingamizi kwenye jambo hilo,” amesema Mashango.

Chrispin Ngushi, amekua na kiwango kizuri tangu alipoanza kuitumikia Mbeya Kwanza FC ambayo inacheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu 2021/22.

Dube, Kangwa, Tigere kuikosa Simba SC
Bumbuli: Hatukupanga kumsajili Sure Boy