Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ameagiza uongozi wa chama hicho kila wilaya kujenga ofisi ifikapo mwaka 2020 na kuondokana na adha ya kupanga.
Ametoa agizo hilo wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la ofisi ya Chadema wilayani Tarime mkoani Mara, ambapo amesisitiza kuwa mpango wa ujenzi wa ofisi hizo ulicheleweshwa na huo haukuwa muda wake.
“Mpango wa ujenzi wa hili jengo umecheleweshwa na huu haukuwa muda wake lakini nawapongeza viongozi walioona njozi ya kuanzisha ujenzi huu ambao uko hatua ya renta ili kuunga mkono ujenzi huu Mimi naanza na Shilingi milioni mbili kila mbunge mkoani Mara achangie milioni moja,”amesema Mbowe
Aidha, hivi karibuni, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Ukonga kupitia chama hicho, Mwita Waitara alimtuhumu mwenyekiti huyo kuwa hela za ruzuku za chama hicho hazieleweki zinakwenda wapi, huku chama hicho kikiwa hakina ofisi makao makuu, Kanda wala mikoani.
Hata hivyo, Mbowe ametoa maagizo hayo wilayani humo ambapo amekwenda kwaajili ya uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Turwa.