Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe ameeleza hatua ambayo vyama hivyo vya upinzani vitachukua katika kuhakikisha kuwa serikali inabadilisha uamuzi wake kuhusu Shirika la Habari Nchini (TBC) kutorusha moja kwa moja (Live) vikao vya Bunge.

Mbunge huyo wa Hai ameeleza kuwa hawataacha kuingia Bungeni baada ya leo kuondolewa kwa nguvu, bali wataendelea kuingia na kudai haki hiyo ya wananchi kupata habari.

Amevitaka vyombo vya habari pamoja na wanaharakati kuunga mkono hatua waliyoichukua ya kupinga hatua hiyo ya serikali.

“Leo tumepaza sauti kwa kelele na sauti kubwa, ili ninyi kama waandishi wa habari kama wadau mcheze nafasi yenu. Waandishi wa habari wa serikali, waandishi wa habari wa kujitegemea, waandishi wa habari wa mashirika binafsi wote mnawajibu katika hili. Hii ni vita ya kitaifa.

“Vilevile asasi nyingine za kiraia na asasi nyingine vilevile huko nje, vitatusaidia kupaza sauti kwamba hili jambo sio sahihi kwa sababu tunaoathirika sio wabunge tulioko bungeni peke yetu bali ni watanzania wote na taifa letu,” aliongeza.

Naye mbunge wa Ubunge, Saed Kubenea na mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya Chadema, Devotha Minja ambao wote ni waandishi wa habari walieleza kuwa kinachotaka kufanyika ni kubana uhuru wa vyombo vya habari na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari.

Leo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alieleza kuwa TBC haitarusha moja kwa moja vikao vya Bunge ili kubana matumizi. Alisema mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye Vikao vya Bunge yatarushwa kupitia kipindi maalum cha ‘Leo Katika Bunge’ kitakachoanza saa nne usiku.

Hata hivyo, Nape amepanga kufanya mkutano na waandishi wa habari kufafanua kauli hiyo ya serikali.

JKU Kupiga Kambi Uganda Kwa Ajili Ya Gabarone United
Yabainika: Habari kuhusu Sheria Mpya ya Eritrea kuoa mke zaidi ya Mmoja au kifungo Sio ya Kweli