Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe jana alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoa Mwanza na kuhojiwa kwa takribani saa mbili katika kituo cha Polisi cha Nyakato katika wilaya ya Nyamagana.

Akizungumza baada ya kutoka katika kituo hicho cha polisi, Mbowe alieleza kuwa alihojiwa na Polisi kuhusu masuala mbalimbali ya chama chake, mahojiano yaliyoongozwa na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Augustine Senga na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana.

Alisema kuwa katika mahojiano hayo, polisi walimtaka kutulia katika hoteli aliyofikia na kwamba asitoke kwenda mahali popote katika jiji hilo bila kuwataarifu polisi, masharti ambayo kwa mujibu wa Mbowe aliyakataa.

“Polisi wamenitaka kuanzia sasa nisitoke hoteli niliyofikia bila kutoa taarifa kwao, hili nimelikataa maana huku ni kutaka kunipa kifungo cha nje kama kiongozi wa upinzani Uganda, Kizza Besigye. Nimewajibu ‘mimi ni kiongozi wa Taifa kama wa CCM, nina haki ya kutembelea ofisi zangu lakini pia kama Mtanzania nina haki ya kutembea popote,” Mbowe anakaririwa.

Mbowe alikamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kuanza kufanya ziara ya kutembelea maskani mbalimbali,  ‘vijiwe’ pamoja na ofisi za chama hicho.

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema kuwa mbali na Mbowe, viongozi wengine wa Chama hicho waliokamatwa na polisi ni Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na Katibu Mkuu ‘Bavicha’, Julius Mwita.

Jeshi la Polisi lilipiga marufuku mikutano yote ya hadhara nchini tanghu Juni 7 mwaka huu kwasababu za kiusalama. Kamishina wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya alisema kuwa wamebaini kuwa mikutano hiyo imelenga kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.

Jeshi la Polisi lamsaka Zitto, lazima kongamano la ACT- Wazalendo
Video: Wabunge wa Ukawa wataka Posho za vikao vya Bunge zifutwe