Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe usiku huu, ikiwa ni saa chache baada ya kesi ya ugaidi dhidi yake kufutwa na kuachiwa huru.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Samia alisema kuwa aliona ni vyema kukutana na Mbowe baada ya kutoka gerezani.
“Ndugu yetu Mheshimiwa Mbowe, leo yuko huru ameachiwa na kutokana na hilo nikaona kuna umuhimu wa kukutana naye ili tuzungumze mawili matatu,” amesema Rais Samia.
“Kikubwa tulichozungumza ni kwamba Tanzania hii ni yetu na wote tunapaswa kushirikiana kuijenga Tanzania, na katika hilo ni muhimu kujenga kuaminiana kwa misingi ya haki. Na kwamba tunaposimamisha misingi ya kuaminiana, kuheshimiana na haki ndipo tutapata fursa nzuri ya kuendesha nchi yetu na kuleta maendeleo ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Naye Mbowe alimshukuru Rais Samia kwa kuridhia kukutana naye na kwa kujali, kwa kuzingatia kuwa alikaa gerezani kwa kipindi cha takribani miezi nane.
Mbowe aliongeza kuwa katika mkutano wao wamezungumzia mambo yaliyokuwa yanakwaza mahusiano mema kati ya vyama vyao.
“Kama alivyosema Mheshimiwa Rais, tumekubaliana msingi mkubwa wa kujenga Taifa letu katika maridhiano na umoja unaokubalika ni kusimama katika misingi ya haki. Na pale haki inaposimama basi na amani inakuwa ‘automatic’,” amesema Mbowe.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA aliongeza kuwa wamekubaliana kuondoa urafiki wa mashaka kati ya vyama hivyo, na kufanya siasa za kistaarabu kuisaidia Serikali kuleta maendeleo na Serikali kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kama chama cha siasa.
“Tumekuwa tuna urafiki wa mashaka kwa muda mrefu na viongozi wa vyama vyetu vikubwa viwili. Tumepitia madhira mengi ambayo hatuhitaji kuyataja tunataka tuvuke hapo twende mbele tufanye siasa za kistaarabu, kuisaidia Serikali kufanya kazi zake vizuri na Serikali nayo kuhakikisha na sisi tunafanya majukumu yetu vizuri, pawe na furaha ambayo Mama (Rais Samia) ameshaanza kuijenga,” amesema Mbowe.
Mbowe amewaomba watanzania kumpa ushirikiano Rais Samia na Serikali yake ili waendelee kuleta maendeleo endelevu.
“Tuko tayari kumpa mama ushirikiano, tunaona watanzania pia wampe mama ushirikiano. Tunapenda maendeleo na tunataka Mama na Serikali yake wasaidie kuyapata hayo maendeleo,” amesema Mbowe.
Mbowe na wenzake watatu wameachiwa huru baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali kuwasilisha nia ya kutoendelea na kesi iliyokuwa ikiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Mbowe alikuwa anashikiwa akikabiliwa na mashtaka ya kupanga njama za kufanya ugaidi.