Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa na mtu mchapakazi aliyekuwa na uthubutu wa kufanya maamuzi magumu.

Mbowe amesema mbali na mambo mengine Hayati Dkt. Magufuli atakumbukwa na mambo makuu mawili na Watanzania wote ambayo ni uthubutu wa kufanya maamuzi magumu pamoja na kusisitiza katika uchapaji wa kazi kwa bidii na kufanya kazi mchana na usiku.

“Hayati Magufuli atakumbukwa kwa mengi mabaya na mazuri, sifa za kipekee za Hayati Magufuli, moja ni uthubutu wa kufanya maamuzi magumu, alikuwa na kipaji hicho nakiita kipaji, la pili aliamini na kusisitiza uchapaji kazi kwa bidii hii ni sifa nzuri,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema, “Rais Magufuli hakuwa mvivu, alijituma alifanya kazi usiku na mchana, alisisitiza Watu wafanye kazi, aliishi Falsafa ambayo CHADEMA tunaiamini kwamba asiyefanya kazi na asile, jambo lile sisi tulilikubali, hapa sijadili Maisha yake binafsi, namjadili aliyekuwa Rais wa Nchi.”

Mbowe ameeleza kusikitika kutokuweza kushiriki mazishi ya Hayati Dkt Magufuli na kutoa pole kwa Familia, ndugu na Watanzania wote.

“Namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai wetu, wapo wengi ambao walikuwa hai mara ya mwisho nilipozungumza na Taifa Mwezi January mwaka huu ambao leo hatunao tena, tumempoteza Rais wetu Dr. Magufuli, nasikitika nilishindwa kurejea nchini kushiriki mazishi” amesema Mbowe.

“CHADEMA ilishiriki katika hatua zote za mazishi ya Hayati Dr. Magufuli chini ya uongozi wa Katibu Mkuu wetu John Mnyika, kwa mara nyingine natoa pole kwa Mjane Mama Janeth Magufuli, Watoto, Ndugu, Familia, Rais na Mama Yetu Samia Suluhu na CCM,” ameongeza Mbowe.

Aidha, Mbowe amemshukuru Rais Samia Suluhu, kwa kwenda kumjulia hali aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu alipopigwa risasi na watu wasiojulikana mwezi Septemba 2017.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mbowe kuzungumza na umma kwa zaidi ya miezi mitatu sasa ambapo ameeleza kuwa hakuwepo nchini kuanzia Disemba 4, 2020 akifanya ziarkatimataifa mbali mbali na shughuli binafsi.

Rais Samia aeleza faida za mradi wa bomba la mafuta
Serikali yatoa tamko watakaopandisha bei ya chakula