Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema hali ya maisha ya Watanzania kwa sasa ni ngumu kuliko awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, amesema kuwa kwa sasa hali ya uchumi kwa Watanzania ni mbaya ukilinganisha na awamu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Shirinjoro kilichopo katika jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, ambapo amesema kuwa uchumi unakuwa katia mifuko ya kikundi cha watu wachache.
Aidha, akihutubia wananchi hao, Mbowe amekilaumu Chama cha Mapinduzi CCM akisema kuwa chama hicho kinatumia vibaya mamilioni ya fedha za walipa kodi ambazo zitatumika katika chaguzi za Kata ambazo madiwani wao walijiuzuru.
“Kama uchumi unakuwa basi unakuwa katika mifuko ya kikundi cha baadhi ya watu wachache, lakini siyo kwa Watanzania tunaowafahamu sisi ambao tuko nao mtaani kila siku,”amesema Mbowe.
Hata hivyo, akizungumza kuhusu madiwani wake watatu waliojiuzuru na kujiunga na CCM, amesema uchaguzi wa marudio katika Kata hizo utatafuna kodi za wananchi kiasi cha shilingi milioni 750.