Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amesema kuwa ziara ya mjumbe wa kamati kuu wa chama hicho Ikulu, Edward Lowassa ilikuwa ziara binafsi na sio ya chama.
Mbowe amesema kuwa ziara hiyo haikuwa na uhusiano na chama na kwamba hakukuwa na ulazima wa kuomba ruhusa katika chama hicho lakini kauli zake za kuisifu Serikali hazikuwa msimamo wa chama.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema kuwa msimamo wa chama sio kuisifu serikali kwani ingawa kuna mambo ambayo imefanya vizuri, mambo ambayo haijafanya vizuri ni mengi kiasi cha kuwafanya washindwe kusimama kuzungumzia mazuri hayo.
“Tungependa mtu mwingine yeyote na sio mheshimiwa Lowassa peke yake, atoke na kauli ya kuipongeza Serikali lakini vilevile aikumbushe Serikali maeneo mengine mengi ambayo imekosea katika kutekeleza wajibu wake,” Mbowe ameiambia Mwananchi.
Hata hivyo, Mbowe amefafanua kuwa chama mtu yoyote atakayekuwa mwanachama akasimama na kutoa kauli ambazo sio msimamo wa chama sio tatizo kwani kila mmoja ana uhuru wa kutoa mawazo yake lakini hayo yatajadiliwa kwenye vikao vya chama inapobidi.