Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, kitafanya maamuzi kwa tahadhari kuhusu kuungana na vyama vingine vya upinzani.

Mbowe ameeleza kuwa wamesikia wito wa vyama vingine vikiwataka kuungana, lakini hawatafanya hivyo kama mtindo tu bali wataangalia maslahi mapana ya chama chao.

Ajira: Nafasi za kazi kwa watangazaji, waandishi wa habari

Aliyasema hayo jana katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, baada ya chama hicho kumpitisha Naibu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 28, 2020.

Lissu aliwashinda waombaji wengine wa nafasi hiyo ambao ni Lazaro Nyalandu na Maryrose Majige.

Kauli hiyo ya Mwenyekiti wa Chadema imekuja siku kadhaa baada ya Chama Cha ACT-Wazalendo ambacho kimempitisha Bernard Membe kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Maalim Seif Sharif Hamad kugombea urais wa Zanzibar, kuomba washirikiane ili waweke mgombea mmoja.

“Chama chetu kitashirikiana na watu ambao ni halisi, wako makini na waliojitolea kweli kumaliza safari nasi pamoja, sio wale ambao watatuacha njiani,” alisema Mbowe.

“Pale tutakapoona inafaa, tutaona uwezekano wa kuunga mkono wagombea wa vyama vingine katika maeneo ambayo Chadema haitakuwa na nguvu kubwa, na zaidi tunaangalia uwezekano wa kutoweka mgombea wa urais Zanzibar,” aliongeza.

Alisema kuwa chama hicho kitaenda kwenye meza ya mazungumzo kuhusu kuungana na vyama vingine vya uchaguzi kikiwa kimeweka mbele maslahi mapana ya nchi na chama.

Mwaka 2015, Chadema iliungana na vyama vingine vinne vya upinzani kuunda Ukawa, umoja ambao ulisambaratika miaka michache baada ya kushindwa uchaguzi wa urais, ingawa ulipata mafanikio makubwa kwa kulinganisha na miaka mingine ya uchaguzi.

Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa alirejea kwenye Chama Cha Mapinduzi miaka michache baadaye.

Waziri Kairuki atembelea maonesho ya Nanenane, akumbusha zabuni kwa makundi maalum

Jeshi lamkamata kigogo wa dawa za kulevya aliyemjaribu Rais
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 4, 2020