Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amezungumzia sakata la kukamatwa kwa mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye ameachiwa leo kwa dhamana.
Mdee alishikiliwa na jeshi la polisi kwa siku tano kufuatia amri ya kukamatwa iliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi baada ya kudaiwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Rais John Magufuli. Mdee emefikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka la kumkashfu Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka mahakamani, Mbowe amesema kuwa Mdee alieleza kuhusu hisia zake na sio vinginevyo kuhusu agizo la Rais Magufuli kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watakaopata ujauzito hawataruhusiwa kuendelea na masomo.
“Sisi kama chama na kama viongozi, tunaamini kila Mtanzania awe kiongozi asiwe kiongozi, wa chama chochote na wa dini yoyote ana haki ya kueleza hisia zake,” alisema Mbowe.
“Halima ni mbunge, ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa (Bawacha). Kwahiyo ni kiongozi mwandamizi, sio tu wanatakiwa waseme anatakiwa akemee. Alipokuwa anazungumza kuhusu watoto kupata mimba alikuwa anazungumza kama mwanamke, Mbunge na Mwenyekiti wa Bawacha,” aliongeza.
Mwenyekiti huyo wa Chadema aliongeza kuwa chama chake kitaendelea na mjadala huo bila kujali hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi yao.