Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amekana kudaiwa kiasi chochote cha fedha na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuahidi kuliburuza mahakamani shirika hilo kwa kuondoa mali zake katika jengo lililoko katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Mbowe imekuja baada ya NHC kuondoa mali zinazomilikiwa na Mbowe katika jengo hilo ikiwa ni pamoja na Club ya Bilcanas na kampuni ya Free Media inayochapisha gazeti la Tanzania Daima, baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nehemiah Mchechu kueleza kuwa Mbowe ni mdeni sugu anayedaiwa shilingi bilioni 1.

“Mimi sidaiwi na NHC,” Mbowe anakaririwa na Mwananchi. “Madai yanayofanyika hayapo kisheria bali ni uharibifu wa makusudi unaolenga kunikomoa kutokana na msimamo wangu wa kisiasa,” aliongeza.

“Kama sio siasa za majitaka, inawezekana  vipi deni hadi lifikie bilioni 1 na kwa kodi ipi nambayo nilitakiwa kulipa kwa mwaka au kwa mwezi?” Alihoji.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kuwa yeye ni mmoja kati ya wana hisa wa jengo hilo tangu mwaka 1997 na kwamba analimiliki kisheria kwa asilimia 75. Hivyo amepanga kulishtaki shirika hilo kwa kile kinachofanyika.

Hata hivyo, Waziri wa Ardh, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema kuwa yeye anachofahamu ni kuwa hakuna ubia katika jengo hilo la NHC na kwamba shirika hilo linachofanya ni biashara na sio siasa.

“Kama Waziri siwezi kuwaingilia NHC lakini najua Mbowe alikuwa anadaiwa na najua pia kuna oparesheni kama hizo kwa wadaiwa wengine sugu,” alisema Lukuvi.

 

 

Rais Magufuli;Ole Wake Atakae Hatarisha Amani Ya Nchi, Asema Hatomvumilia Mtu, Aagiza Vyombo Vya Dola Kuanza Kuwashughulikia
Video: Waziri Mkuu atembelea kituo cha tiba cha kimataifa (MUHAS)