Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu wameandikiwa barua na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wakitakiwa kujieleza kwa matamko yao waliyoyatoa katika siku za hivi karibuni.

Lissu amekiri kupokea barua kutoka kwenye Sekretarieti hiyo akieleza kuwa imeandikwa na Jaji mmoja mstaafu ambaye hata hivyo hakumtaja jina.

“Ni kweli mimi na Mwenyekiti Mbowe tumepata barua hiyo. Ni barua ya ajabu ambayo imeandikwa na mtu aliyewahi kuwa Jaji wa mahakama kuu,” Lissu anakaririwa na Mwananchi. “Sitaki kuzungumza mengi kwa sasa, Jumatano nitalizumzia vizuri jambo hili,” aliongeza.

Hata hivyo, Kamishna wa Sekretarieti, Jaji Mstaafu Salome Kaganda alieleza kutofahamu chochote kuhusu barua hiyo iliyodaiwa kuwafikia viongozi hao wa Chadema.

“Mimi sifahamu kuhusu suala hilo, sina taarifa,” Jaji Kaganda alimueleza mwandishi wa gazeti hilo.

Hata hivyo, hali hiyo imeibua maswali kwani viongozi hao wa siasa ambapo pia ni wabunge, hawana sifa za kuwa watumishi wa umma na hakuna kiapo cha utumishi wa umma kinachowabana.

Mbowe na Lissu walihojiwa hivi karibuni na Jeshi la Polisi kutokana na matamshi yao wakati wa kutangaza Operesheni UKUTA. Lissu anadaiwa kutoa kauli za kichochezi na kuidharau mahakama.

 

 

Rasmi - John Stones Asajiliwa Etihad Stadium
Jina La Stones Laonekana UEFA Kama Mchezaji Wa Man City