Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Katavi (CCM), Martha Maliki amechangia mabati bando tano zenye thamani ya shilingi milioni 2.4 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Shule ya Kiislam ya Sheikh Aboubakar Zuberi Pre & Primary school inayojengwa na BAKWATA mkoa wa Katavi.

Makabidhiano ya mchango huo, yamefanyika katika msikiti Mkuu wa Ijumaa mjini Mpanda na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Baraza la Waislam (BAKWATA) wakiongozwa na sheikh Mkuu wa Mkoa huo sheikh Mashaka Kakulukulu.


Akizungumza mara baada ya kukabidhi mabati hayo, Malick amesema amewaomba wadau wengine kuendelea kujitoa katika kuchangia shule hiyo kwani haitawanufaisha waislam pekee bali watanzania wote na kuongeza kuwa kitendo hicho ni moja ya jitihada za kumuunga mkono Rais wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Kwa upande wake, Sheikh Kakulukulu amemshukuru Mbunge huyo kwa moyo wa kujitoa alionao na kumuahidi kuendeleza ushirikiano baina ya viongozi wengine ili kuweza kutimiza azma ya ujenzi wa Shule hiyo.


Sheikh Kakulukulu amesema, pindi itakapo kamilika shule hiyo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi wa elimu ya awali na elimu ya msingi na baadae upo mpango wa kuiongezea uwezo kuanza kupokea wanafunzi wa sekondari.

Martha Malick, anakuwa Mbunge wa pili kuchangia ujenzi wa Shule hiyo baada ya Mbunge wa jimbo la Mpanda Kati Simon Kapufi kufanya hivyo mwanzoni mwa ujenzi wa Shule hiyo.

Shule ya Sheikh Aboubakar Bin Zuberi inakuwa shule ya kwanza kumilikiwa na Baraza la waislam (BAKWATA) mkoani Katavi na inategemewa kuwa chachu ya elimu katika mkoa huo.

Iringa kufanya utafiti tatizo la utapiamlo
Vyombo vya Habari ‘kuanzisha’ dawati la jinsia