Mbunge wa Tabora mjini Emmanuel Mwakasaka, amesema wakinamama wanaokwenda kujifungua katika Hospitali ya Kitete mkoani Tabora wamekuwa wakitozwa kati ya Sh 30,000 hadi Sh 50,000 wakati wakijifungua kawaida.
Akiuliza swali hilo bungeni leo Februari 5, 2020, Mwakasaka amesema licha ya uwepo wa sera wa huduma hiyo kuwa bure na kauli za viongozi lakini bado inatoza fedha.
Aidha amehoji ni nini msimamo wa Serikali katika jambo hilo kwasababu wale wanaoshindwa kutoa kiasi hicho cha fedha wamekuwa wakizuiliwa hadi watoe fedha hizo wao na watoto wao wanapofika katika hospitali hiyo wakati wa kujifungua.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel amesema msimamo wa Serikali umeweka sera kuwa matibabu ya wanawake hao wanaojifungua bila kutoa fedha.
Hata hivyo, amewataka waganga wakuu wahakikishe wanasimamia suala hilo.
Amesema hospitali hiyo hukusanya hilo Sh73 milioni gharama za matibabu, Sh133 milioni za Bima ya Afya na Sh34 milioni kutoka Serikalini na hivyo kuwa na Sh260 milioni kwa mwezi.
Amesema Sh13 milioni ni matumizi yanayotokana na huduma zinazotolewa bure ikiwemo wanawake wanaojifungua na Sh134 milioni kwa ajili ya matumizi mengine na hivyo kubakiwa na Sh120 milioni.
Amesema hakuna sababu ya kumtoza mama fedha wakati wa kujifungua kwasababu wameshalipiwa gharama hizo.