Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe mkoani Njombe, Mhandisi Gerson Lwenge ametoa wito kwa wananchi mkoani humo kuacha kuuza kiholela mazao ya chakula hususani mahindi ili kuondokana na baa la njaa.

Lwenge amesema kuwa mwaka jana soko la mazao hususani mahindi lilikuwa limeyumba ukilinganisha na mwaka huu hivyo baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakiongezeka mkoani Njombe kufuata mahindi.

“Mwaka jana tumeyumba sana kwenye soko la mazao hasa mahindi, lakini mwaka huu bei ni nzuri na inaendelea kupanda, maeneo mengine kwenye nchi hii hakuna mahindi ndio maana wote wanakimbilia Njombe, sasa nitoe angalizo tuwe waangalifu kwenye eneo la kuuza mahindi mwaka huu ili tusiwe na Njaa,”amesema Lwenge

Aidha, kuhusu suala la Mbolea na pembejeo ambalo limelalamikiwa na wananchi wa kijiji hicho, Lwenge amesema kuwa serikali imejipanga kuleta bei elekezi na nafuu badala ya kutoka kwa walanguzi ambapo walikuwa wakinufaika wachache.

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Igima, Paulina Samatta amesema kuwa bei ya zao la mahindi kwa kata hiyo limekuwa kubwa huku bei zikifikia shilingi 7000 kwa debe moja na kuungana na mbunge wa jimbo la Wanging’ombe kuhamasisha wananchi kuwa waangalifu katika biashara ya zao hilo la chakula.

“Mahindi katika kata yangu tumepata kwa wingi lakini bei pia zimefumuka,sasa hivi debe moja walanguzi wamepita wananunua mpaka shilingi 7000, na mimi ninahamasisha wananchi kutulia kwasababu kama tutauza mahindi yote tunaweza kuingia kwenye Njaa,”amesema Samatta

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Lulanza akiwemo Fredy Kilasi na Blasto Mpolya wamekiri kupanda bei kwa zao hilo na kuongezeka kwa wateja huku wakiahidi kutekeleza wito wa mbunge huyo.

Fanyeni utafiti kwanza kabla hamjatoa habari nyeti- Dkt. Tulia Ackson
Tanzania kuendelea kunufaika na SADC