Operesheni ya kuhakikisha serikali inapata mapato ya kutosha kwa ajili ya kuwaletea wananchi wake maendeleo imeendelea kuzua hoja mbalimbali Bungeni. Jana, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alitoa hoja ya aina yake itakayoongeza njia za serikali kupata mapato.

Akitoa mchango wake kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2016/17, Keissy aliitaka Serikali Kuu kuziruhusu Serikali za Mitaa kukusanya kodi za mifugo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mbwa lakini pia baiskeli zilipiwe kodi.

“Mtu ana ng’ombe 300,000 ana ng’ombe 30,000 halipi kodi. Mifugo ilipe kodi. Nyie mmechukua properties za nyumba ndugu zangu, kwahiyo na nyie Halmashauri wapeni wadai kodi za mifugo… wadai kodi za mbwa, wadai kodi za baiskeli,” alisema Keissy.

Kadhalika, Mbunge huyo alishauri panga la kodi lipitie pia kwenye michango mbalimbali na harambee ikiwa ni pamoja na michango ya misiba, harusi na kile kinachotolewa na waumini katika nyumba za ibada kama sadaka.

“Michango ya harusi, harambee za vyama, harambee za vyama, harambee za harusi na yenyewe idaiwe kodi. Michango ya misiba tunaona mikubwa hata humu Bungeni mhehimiwa naibu spika, nayo ikatwe kodi. Wabunge wanachanga hadi shilingi 100,000 kwa misiba, idaiwe kodi. Hatuwezi kusamehe kodi. Kila shilingi 100,000 idaiwe shilingi 18,000. Sadaka idaiwe kodi,” Mbunge huyo wa Nkasi Kaskazini anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo alieleza kushangazwa na kitendo cha baadhi ya wabunge kutetea makampuni ya migodi na makampuni ya simu kuhusu malipo ya kodi. Alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona kuwa hata Rwanda ambayo ni nchi ndogo inaizidi Tanzania kwa kukusanya kodi inayotokana na matumizi ya mawasiliano ya simu.

Victor Wanyama Amfuata Mauricio Pochettino Jijini London
Rais Wa Paris St Germain Amfuta Kazi Laurent Blanc