Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoani Pwani, Hamoud Jumaa ametoa mabati 60 kwa ajili ya kuezeka darasa moja chakavu katika shule ya msingi Magindu.
Aidha amekabidhi shil. milioni mbili ambayo imenunuliwa bati 56 zitakazotumika kuezeka darasa jingine moja kati ya madarasa manne chakavu kimiundombinu yaliyopo shuleni hapo.
Jumaa amechangia pia matofali 1,000 na mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kata ya Boko kijiji cha Mpiji.
Akikabidhi mabati hayo kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Magindu, Kasule Ambogo, mbunge huyo amesema anatekeleza ahadi alizozitoa na kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuboresha na kutatua changamoto za sekta ya elimu.
Hata hivyo ,amekabidhi mabati mengine 25 yanayokwenda kutumika kuezeka ofisi ya walimu shule ya msingi Muungano Kata ya Kilangalanga.
“Tumefanya harambee kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika Kata ya Boko kijiji cha Mpiji ambapo tumepata shil milioni 7, tofali 5,274, Kokoto gari tatu, mchanga gari moja na mawe gari saba,”amesema Jumaa.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Kilangalanga, Mwajuma Denge amesema kuwa haijawahi kutokea Mbunge wa kuwashika mkono kwa namna hiyo kwa muda wote.